Rais Mustaafu Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aendelea na ziara yake Mjini Goma, Kivu Kaskazini, ambako waliwasili tangu tarehe ishirini na tano iliyopita. Kabila aliwasili baada ya Bunge kumuondolea kinga kwa tuhuma za kushirikiana na uasi wa AFC/M23.
Kabila amekutana na kuendesha mazungumzo na watu mbali mbali, ikiwemo makanisa, viongozi wa kimila, wakuu wa vyuo vikuu, wanawake, wawakilishi wa makabila mbali mbali, pamoja na viongozi wa waasi wa AFC/M23, diaspora kutoka Ulaya, na kwa sasa wanasiasa wa DRC walio uhamishoni, kama vile gavana wa zamani Cishambo.
Lengo kubwa ni kufahamu tatizo na suluhu kwa mzozo wa mashariki mwa Congo, mzozo ambao umepelekea watu wengi kufariki dunia na wengine kuwa wakimbizi katika taifa lao. Idadi kubwa ya walio kuwa katika kambi pambezoni mwa Mji wa Goma wamerudi tayari nyumbani, yaani katika vijiji vyao.
Viongozi wa kimila na wanawake wameomba Joseph Kabila kuchangia swala la amani na usalama kwani sasa wananchi wa Congo, hasa eneo la mashariki, wamechoshwa na vita vya mara kwa mara. Kabila amekuwa akifanya mikutano nyumbani kwake kuelewa na kusikiliza wananchi ambao wanalalamikia hali ya maisha, ikiwemo ukosefu wa benki na maisha magumu.