Raia wengi wakimbilia katika Mji wa Uvira kuhofia maisha kutokana na mapigano katika vijiji vya KIGONGO–KATONGO–KABIMBA COOPELA.
Taarifa zasema raia mmoja huenda amefariki dunia kutokana na mlipuko wa bomu wakati wa mapigano kati ya AFC/M23 na vikosi vya jeshi la serikali linaloungwa mkono na wazalendo, Jumamosi Desemba ishirini na saba, katika kijiji cha Kigongo kilicho umbali wa kilometa saba kusini, nje kidogo ya mji wa Uvira, Kivu Kusini mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa vyanzo vya raia.
Mapigano hayo yamesababisha wakazi wa vijiji vya Kigongo, Katongo na Kabimba katika Almashauri ya Kalungwe, Usultani wa Bavira, kuhama makazi yao kutokana na hali ya kiusalama.
Walio wengi wamekimbilia mjini Uvira na wachache Makobola kutokana na milio ya risasi.
Mapigano kwa sasa yamesimama kidogo baada ya wazalendo na FARDC kurudi nyuma hadi maeneo ya Makobola, ameieleza mwananchi mmoja wa kijiji cha Katongo aliyeshuhudia mapigano hayo.
Huku wananchi wa maeneo hayo wakiomba usalama wa kudumu badala ya milio ya risasi ya mara kwa mara, wakaazi wengi wanaomba suluhisho la haraka kwa mzozo wa DRC ambao umesababisha wengi kuwa wakimbizi.
Taarifa za sasa zasema M23 imefanikiwa kuwasogeza nyuma FARDC na washirika wao kwa ajili ya ulinzi wa Mji wa Uvira.
Jumapili hii Desemba 28, makanisa mengi ya Kikristo yamekusanyika kwa uoga, wachache wakishindwa kumwabudu Mungu Mwenyezi Mungu kutokana na wasiwasi.
Siku chache zilizopita, M23 ilijitangaza kuondoka mjini Uvira kwa shinikizo la Marekani, huku serikali ya Kinshasa ikisema ni uongo kutokana na ripoti za raia waliopo Uvira wanaodai kuona vikosi vya M23. Bisimwa alisema kuondoka kwa M23 ni mchakato, na maandamano mengi kwa sasa yanafanyika hapa na pale kuomba M23 kubaki Uvira.