Utawala wa FARDC na wazalendo huko Makobola umepiga marufuku usafiri wa boti na meli katika Ziwa Tanganyika kutoka Uvira, mji unaosemekana kuwa bado unaokaliwa na M23, tuhuma zinazotupiliwa mbali na AFC/M23 kwenda Baraka.
Akizungumza na vyombo vya habari, Waubwela Mwila Dalton, msemaji wa Yakotumba na wazalendo wa Kivu Kusini, ameweka mkazo kuwa katazo hilo limeanza Jumatatu, Januari 10.
Aliongeza kuwa boti yoyote itakayokamatwa wakati wa doria itakuwa chini ya ulinzi wao na kutumika katika shughuli za usafirishaji wa askari.
Upande wao wamesema kuwa hatua hiyo ni njia ya kulinda usalama wa mji wa Baraka kwa kuhofia kuingia kwa M23 katika mji huo.
Usalama mdogo umepelekea kuibuka kwa njaa na magonjwa ya kipindupindu katika miji ya Uvira na Baraka.
Usafiri wa boti ulikuwa ukirahisisha mzunguko wa bidhaa kwa kupunguza janga hilo, wamesema wamiliki wa maboti.
Akizungumza na MTV, Oscar Balinda, msemaji wa M23, amesema kuwa vikosi vyao haviko katika mji wa Uvira bali ni propaganda za Kinshasa zinazolenga kuwachafua.
Balinda amesema wao hawataki uwepo wa FARDC na wazalendo mjini humo, bali vitumwe vikosi visivyoegemea upande wowote.
Haya yanajiri wakati ambapo operesheni za kivita kati ya jeshi la DRC linalosaidiwa na wazalendo dhidi ya M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mujibu wa Kinshasa na Umoja wa Mataifa, bado zinaendelea huko Kigongo, upande wa Uvira, Kivu Kusini mashariki mwa DRC.