Wakaazi wa Mji wa kibiashara wa Butembo Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC wakabiliana na uhaba wa maji.
Maji ikiwa muhimu kwa maisha ya mwanadamu, wakaazi wa kata mbalimbali zinazo unganisha Mji wa Butembo wanalazimika kuamka saa tisa za usiku kutafuta maji kwa ajili ya familia zao. Wengi hufanya safari ndefu usiku kutafuta maji kwenye visima, huku wengine wakipitia mabonde na sehemu hatarishi ili kupata maji.
Wakaazi wa Mji wa Butembo wamekuwa wakishutumu kwa muda mrefu shirika la REGIDESO kwa kushindwa kuwafikishia maji kwa kipindi kirefu. Mji wa Butembo una milima, mabonde na maeneo ya miinuko (tingitingi) yanayofanya usambazaji wa maji kuwa changamoto.
Kutokana na ukosefu wa maji, wakaazi wengi wameamua kuchimba visima vyao binafsi. Hata hivyo, baadaye hukumbana na usumbufu wa serikali wa kuwataka walipe kodi, licha ya kutumia pesa zao wenyewe kutafuta maji kutokana na uzembe wa serikali yenye wajibu wa kuwapatia wakaazi huduma muhimu kama maji, umeme, barabara, shule, vituo vya afya na huduma nyingine.
Jumatatu hii MTV imetembelea kata ya Vuhira kilometa nne eneo la Bulengera na kukutana na mama mmoja aliyeripoti hali mbaya wanayopitia wakaazi katika harakati za kutafuta maji, hasa baada ya bomba la Muleka kukauka maji, ambalo ndilo lilikuwa linawasaidia awali.
Mji wa Butembo una idadi kubwa ya wakaazi pamoja na wakimbizi wa ndani waliokimbia vijiji mbalimbali kutokana na mauaji ya ADF na vita kati ya M23 na jeshi la serikali kusini mwa wilaya ya Lubero. Kwa sasa, wengi wao wanapatikana mjini bila msaada wa kutosha na wanaendelea kupitia hali ngumu ya maisha.
Kwa sasa, sehemu ya wakaazi wa wilaya ya Vulamba na Mususa wanatumia maji kutoka kisima cha Vuhesi, ambacho kimegawanywa katika kata mbalimbali kupitia msaada wa shirika moja lisilo la kiserikali. Wakaazi wanaomba serikali kutafuta suluhisho la kudumu kwa kujenga bomba jingine la maji katika Mji wa Butembo.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa mabomba (pipeline) yanayobeba maji katika Mji wa Butembo ni ya zamani na kwa sasa yana uchafu, hali inayoweza kuwa chanzo cha magonjwa. Aidha, wakati wa mvua, maji yanayotumika mjini huwa machafu zaidi kutokana na uangalizi duni wa mifumo ya maji inayosimamiwa na wafanyakazi wa serikali.