Vijana kutoka makundi mbali mbali katika mji wa kibiashara wa Butembo waandamana wameitisha mgomo wa kutofanya kazi hii juma nne tarehe 13 January 2026 kuomba usalama wa wananchi na viongozi kuwajibika.
Tangu asubuhi, kazi za usafiri na kibiashara zilisitishwa hadi saa za tano za mchana katika maeneo ya Furu na Mutsanga kaskazini mwa mji wa Butembo, huku baadhi ya shule zikishindwa kufungua milango yake kutokana na hofu ya kushambuliwa na waandamanaji.
Wafanya biashara katika mji wa Butembo wamechukulia kwa shingo upande hatua ya vijana kuitisha mgomo bila kushirikisha wadau wengine, wakati mji wa Butembo unategemea biashara. Polycarpe Ndivitho, kiongozi wa shirika la FEC, aliomba vijana kutafuta njia nyingine za mgomo badala ya maandamano, akisema maandamano yanaweza kusababisha vurugu na uporaji wa mali.
Ndivitho alisema kuwa migomo ya mara kwa mara huyumbisha uchumi wa wakaazi wa Butembo.
Mji wa Butembo kwa sasa unapokea wakaazi wengi wanaohama makazi yao kutokana na ukosefu wa usalama katika vijiji mbalimbali kufuatia mashambulizi ya ADF na vita vya M23. Wakaazi wengi wanaishi kwa pato la kila siku, huku vijana wa Butembo wakishutumu uongozi wa kijeshi wa eneo hilo kwa kushindwa kuwalinda raia