DRC

Wakaazi Wa Mwenye wilayani Lubero walalamikia hali mbaya ya usalama unao tokana na mauaji inayo tekelezwa na watu wanao dhaniwa kuwa ADF

JANUARI 25, 2026
Border
news image

Mkaazi mmoja alie hifadhi jina lake asema usiku wa Juma Mosi, Januari 24, 2026, shambulizi jipya kutoka watu wenye silaha wanaodhaniwa kuwa ADF lililenga kijiji cha Musenge/Mbata, eneo la Mwenye katika usultani wa Baswagha, wilayani Lubero, Kivu Kaskazini.

Taarifa zasema kuwa watu wenye silaha walishambulia kijiji hicho tangu saa mbili za usiku na kusababisha hali ya wasiwasi kwa wakaazi, ambao wengi walitembea safari ndefu kwa miguu wakihofia maisha yao na kuelekea maeneo yenye usalama zaidi, hasa Butuhe kaskazini mwa mji wa Butembo.

Hadi sasa idadi kamili ya maafa haijajulikana kutokana na kila mmoja kukimbia kuokoa maisha yake. Wakaazi wengi wameacha makaazi yao baada ya nyumba zao kuchomwa moto, ikiwemo jengo la kanisa Katoliki.

Shambulizi la kijiji cha Musenge ni mfululizo wa mashambulizi yaliyopelekea zaidi ya watu ishirini na tano kuuawa, nyumba 56 na pikipiki mbili kuchomwa moto, huku mtu mmoja akijeruhiwa vibaya katika vijiji tofauti vya Mwenye tangu mwanzoni mwa juma tatu lililopita.

Wakaazi wanalalamikia mashambulizi yanayoongezeka kasi katika eneo la Mwenye, huku viongozi wa mkoa wakitajwa kuwa katika mji wa Beni, eneo la karibu na tukio. Maelfu ya wakaazi, hasa wakulima, wamehama makaazi yao tangu mwaka uliopita kutokana na tishio la ADF.

Wakaazi wa Baswagha na Bapere, ambao wengi ni wakulima na wachimba madini, wapo katika hatari ya kukumbwa na utapiamlo baada ya mashamba yao kuvamiwa na makundi yenye silaha.

Abel Tsongo - MTV1 Online