Watu wenye silaha wanao dhaniwa kuwa ADF walieshambulia vijiji vitatu kilometa tano kaskazini mwa Manguredjipa wilayani Lubero, Kivu Kaskazini, hii ikiwa mfululizo wa mashambulizi na mauaji ya raia wasio na hatia.
Mashambulizi haya mabaya yameripotiwa hii Alhamisi, Oktoba thelathini, elfu mbili ishirini na tano. Wapiganaji kutoka kundi la kigaidi la ADF walishambulia wakulima katika mashamba ya Malewe, Pethema na Pangoy, eneo la uchimbaji madini muhimu kwa ajili ya kusaidia wakaazi, na kulazimisha watu kukimbia kwa mara nyingine japo eneo hilo lilipokea maelfu ya watu kutoka katika vijiji mbali mbali wakiogopa mauaji katika sekta ya Bapere ambayo kwa sasa yaandamwa na mauaji kila siku.
Wapiganaji hao walishambulia pia ngome la wapiganaji wazalendo lililowekwa kwa ajili ya kulinda doria eneo za Pangoy kwa usalama wa wachimba madini, na kuchoma kwa moto nyumba zilizojengwa kwa mbao na kuteka watu wengi ikiwemo watoto wenye umri mdogo. Baada ya shambulizi, mwili mwingine wa mchimba madini uligunduliwa Mandala kwenye barabara ya Manguredjipa_Fatua.
Wakaazi waishio upande wa kaskazini mwa Manguredjipa wanaishi hali ya wasiwasi, wengi wao wakilazimika kuhama na kukimbilia eneo la usalama hasa Manguredjipa na vijiji vingine. Kwa sasa, ni vigumu kupata taarifa zaidi kutokana na kwamba wakaazi wengi wamehama vijiji na kukimbia.